Kile tunachokiamini na kile tusichokiamini

KUHUSU SHEKINAH NA PRESBYTERIAN

Kabla ya kuanza kueleza mafundisho, utaratibu, au mwelekeo wa kanisa, ni jambo la msingi kabisa kuelewa maana ya jina linalolitambulisha kanisa. Katika maandiko, jina halikuwa tu utambulisho wa kawaida, bali lilihusishwa na kusudi, tabia, na ufunuo wa Mungu. Vivyo hivyo, jina la kanisa hubeba tamko la imani na dira ya kiroho. Kwa hiyo, kuelewa maana ya neno Shekinah ni hatua ya kwanza ya kuelewa moyo na mwelekeo wa Shekinah Presbyterian Church.

Neno Shekinah lina asili yake katika lugha ya Kiebrania, likitokana na mzizi shakan unaomaanisha kukaa, kutua, au kukaa katikati ya watu. Katika fikra za Kiyahudi, Shekinah lilitumika kuelezea uwepo wa Mungu unaokaa kati ya watu wake kwa namna halisi na inayotambulika. Ingawa neno Shekinah halionekani moja kwa moja katika maandiko ya Biblia kama neno lililoandikwa, dhana yake imejaa kwa kina katika simulizi za Biblia, hasa katika Agano la Kale. Hili ni jambo la kawaida katika theolojia, ambapo neno hutumiwa baadaye kuelezea ukweli ambao maandiko yanafundisha kwa wazi.

Katika Agano la Kale, Mungu anajifunua kama Mungu anayekaa na watu wake, si Mungu wa mbali au wa kufikirika. Uwepo wake unaonekana kwa ishara za utukufu. Katika Kutoka 24:16 Biblia inasema, “Utukufu wa Bwana ukakaa juu ya mlima Sinai, na lile wingu likaufunika muda wa siku sita.” Kauli ya “ukakaa” inaonesha wazi dhana ya Shekinah, yaani Mungu kutua mahali fulani kwa utukufu wake.

Uwepo huu wa Shekinah unaonekana pia katika Hema ya Kukutania. Kutoka 40:34 inasema, “Ndipo lile wingu likalifunika hema ya kukutania, na utukufu wa Bwana ukaijaza ile maskani.” Hapa tunaona Mungu akichagua kukaa katikati ya watu wake, akiwaongoza, akiwaokoa, na akiwaweka chini ya uwepo wake mtakatifu. Vivyo hivyo, wakati wa kuwekwa wakfu kwa Hekalu la Sulemani, maandiko yanasema, “Makuhani walipotoka patakatifu, lile wingu likajaza nyumba ya Bwana… maana utukufu wa Bwana uliijaza nyumba ya Bwana” 1 Wafalme 8:10 hadi 11. Shekinah hapa inaonekana kama uwepo wa Mungu unaotawala na kuhitaji heshima, kiasi kwamba huduma ilisimama kwa sababu ya utukufu wa Mungu.

Hata hivyo, Agano la Kale pia linaonesha kwamba Shekinah ya Mungu haikaa mahali penye dhambi bila toba. Katika Ezekieli 10, nabii anaona utukufu wa Bwana ukiondoka hekaluni kwa sababu ya uasi wa watu. Hili linafundisha kwamba uwepo wa Mungu unahusiana moja kwa moja na utii, utakatifu, na uaminifu wa agano.

Katika Agano Jipya, dhana ya Shekinah haifutwi bali inatimia kikamilifu ndani ya Yesu Kristo. Yohana 1:14 inasema, “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake.” Neno “akakaa” hapa lina maana ya kukaa hemani. Hii inaonesha kwamba Yesu Kristo ndiye Shekinah iliyo hai. Mungu hakukaa tena katika wingu au jengo, bali katika mwili wa mwanadamu, akitembea kati ya watu, akizungumza nao, na kuwakomboa.

Baada ya Kristo kupaa mbinguni, maandiko yanafundisha kwamba Shekinah ya Mungu sasa inakaa ndani ya waamini kupitia Roho Mtakatifu. Kanisa linaelezwa kuwa hekalu la Mungu. 1 Wakorintho 3:16 inasema, “Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?” Hapa Shekinah inahama kutoka mahali maalumu kwenda kwa jumuiya ya waamini. Uwepo wa Mungu sasa unakaa ndani ya watu waliokombolewa, na kwa pamoja wanakuwa maskani ya Mungu.

Kwa hiyo, jina Shekinah linatangaza imani katika Mungu anayekaa na watu wake. Linatukumbusha kwamba kanisani  ni mahali pa kukutana na uwepo halisi wa Mungu. Linatuita kuishi maisha ya utakatifu, unyenyekevu, na utiifu, kwa sababu Mungu anakaa katikati ya watu wake.

Hapa ndipo tunapounganisha jina Presbyterian. Neno Presbyterian linatokana na neno la Kigiriki presbyteros linalomaanisha mzee (siyo kwa umri). Katika Agano Jipya, kanisa liliongozwa na wazee waliowekwa kwa msingi wa wito, tabia, na mafundisho sahihi. Mfumo wa Presbyterian unatilia mkazo uongozi wa kibiblia na usimamizi wa pamoja, uwajibikaji, na utaratibu wa kibiblia katika maisha ya kanisa. Ni mfumo unaolinda kanisa dhidi ya mtu mmoja kuwa na mamlaka yote, na badala yake kuhimiza uongozi wa pamoja chini ya Kristo aliye kichwa cha kanisa.

Uzuri wa mfumo wa Presbyterian ni kwamba unaheshimu utaratibu, nidhamu, na uwajibikaji wa kibiblia, huku ukitambua kwamba mamlaka ya mwisho ni Neno la Mungu. Ni mfumo unaothamini mafundisho sahihi, maamuzi ya pamoja, na uongozi unaohudumia, si unaotawala kwa mabavu.

Kwa hiyo, Shekinah Presbyterian ni muunganiko wa kina wa kweli mbili za kibiblia. Shekinah inatangaza uwepo wa Mungu unaokaa katikati ya watu wake. Presbyterian inatangaza namna ambavyo watu hao wanaishi chini ya uongozi wa kibiblia, wenye utaratibu, uwajibikaji, na heshima kwa Neno.

Shekinah Presbyterian Church, kwa hiyo, ni jumuiya inayotamani uwepo wa Mungu unaokaa kati yao, na wakati huo huo inajenga maisha ya kanisa juu ya msingi wa uongozi wa kibiblia, mafundisho sahihi, na ushirika wenye nidhamu. Ni kanisa linalotambua kwamba bila Shekinah, utaratibu hubaki kuwa mfumo mtupu. Na bila utaratibu wa kibiblia, hamu ya uwepo wa Mungu inaweza kupoteza mwelekeo.

A. KUHUSU MAFUNDISHO

1. Kuhusu Maandiko Matakatifu

Tunaamini Maandiko Matakatifu ni ufunuo wa Mungu ulioandikwa, uliovuviwa na Roho Mtakatifu, na ndiyo mamlaka ya juu kabisa katika imani, mafundisho, mwenendo, na utendaji wa kanisa. Tunaamini Biblia yote, kuanzia Mwanzo hadi Ufunuo, ni Neno la Mungu lililo hai, la kweli, na la kutosha kwa wokovu na kwa maisha ya kumpendeza Mungu.

Tunaamini ufunuo huu haukutokana na hekima ya kibinadamu wala uzoefu wa wanadamu peke yao, bali “hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.” (2 Petro 1:20–21). Hii ina maana kwamba ingawa Mungu aliwatumia waandishi wa kibiblia wenye historia, lugha, na mazingira tofauti, Roho Mtakatifu ndiye aliyesimamia ujumbe ili usipotoshwe, bali uwasilishwe kwa uaminifu.

Tunaamini Maandiko Matakatifu hayana makosa katika kusudi lake la kumfunua Mungu na mpango wake wa wokovu. Kwa hiyo, Biblia ni ya kuaminiwa katika yote inayofundisha kuhusu Mungu, dhambi, wokovu, maadili, na tumaini la milele. Kama Paulo alivyofundisha, “kila andiko lenye pumzi ya Mungu lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki, ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema” (2 Timotheo 3:16–17). Aya hii inaweka wazi kuwa kazi ya Maandiko si kutupa maarifa tu, bali kutubadilisha na kutuandaa kwa maisha ya utiifu.

Tunaamini Maandiko Matakatifu yanajitafsiri yenyewe, na Yesu Kristo ndiye ufunguo wa kuyafahamu. Tunafundisha kwamba Biblia yote inaelekeza kwa Kristo, kazi yake ya ukombozi, na ufalme wake. Kama Yesu mwenyewe alivyowaeleza wanafunzi wake, alianza “katika Musa na manabii wote, akawaeleza katika maandiko yote yaliyomhusu yeye” (Luka 24:27). Kwa hiyo, katika mafundisho na mahubiri yetu, tunatafuta kueleza maana ya andiko katika muktadha wake, kisha kulielekeza kwa Kristo na kulihusisha na maisha ya waamini leo.

Tunaamini Maandiko Matakatifu yanatosha. Hii ina maana kwamba hakuna ufunuo mpya unaoweza kulingana au kupingana na Biblia. Tunathamini sana karama za Roho Mtakatifu, maongozi, na mafunuo ya kiroho, lakini tunaamini mambo yote hayo yanapaswa kupimwa kwa Neno la Mungu. Kama kanisa, tunasimama katika msimamo wa mitume uliotamka wazi kwamba hata malaika akihubiri injili tofauti na ile iliyokwisha kufundishwa, ahesabiwe amelaaniwa (Gal. 1:8–9).

Tunaamini Maandiko Matakatifu ni msingi wa umoja wa kanisa. Umoja wetu haujengwi juu ya hisia, desturi, au tamaduni, bali juu ya ukweli wa Neno la Mungu. Ndiyo maana tunahimiza kila mshirika asome Biblia binafsi, aitafakari, na aitii, akitambua kwamba kukua kiroho hakutokani na kusikiliza mahubiri tu, bali pia na kuishi chini ya mamlaka ya Neno kila siku. Kama mtunga Zaburi anavyosema, “neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu” (Zab. 119:105).

Kwa hiyo, kama kanisa, tunakiri wazi kwamba hatuwezi kuishi, kufundisha, wala kuhudumu kwa uaminifu bila Maandiko Matakatifu. Tunayapokea kwa heshima, tunayafundisha kwa uaminifu, tunayatafakari kwa unyenyekevu, na tunajitahidi kuyaishi kwa msaada wa Roho Mtakatifu, ili Mungu atukuzwe na watu wake wajengwe katika imani ya kweli.

2. Kuhusu Utatu

Tunaamini Mungu ni mmoja, wa kweli na wa milele, aliye juu ya vyote, asiye na mwanzo wala mwisho, na anajifunua katika nafsi tatu, Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Tunaamini hawa watatu si miungu watatu, bali ni Mungu mmoja katika uungu mmoja, utukufu mmoja, na asili moja. Nafsi hizi tatu zinatofautishwa kwa uhusiano na utendaji wao, lakini hazitenganishwi katika uungu wao.

Tunaamini Baba ni Mungu, chanzo cha vitu vyote, mpaji wa uhai, na mtimizo wa mapenzi yake katika historia. Tunaamini Mwana, Yesu Kristo, ni Mungu kweli, Neno aliyefanyika mwili, aliyekuwepo tangu mwanzo pamoja na Mungu, na ambaye kwa yeye vitu vyote vilifanyika (Yohana 1:1–3, 14). Yesu hakuwa kiumbe aliyeumbwa, bali ni wa milele, sawa na Baba kwa uungu, naye alipata mwili kwa ajili ya wokovu wetu. Ndani yake, Mungu alijifunua kwa namna kamili na inayoonekana kwa wanadamu.

Tunaamini Roho Mtakatifu ni Mungu, nafsi ya tatu ya Utatu, atokaye kwa Baba, naye hutumwa na Baba na Mwana kwa ajili ya kutekeleza kazi ya Mungu katika mioyo ya waamini. Tunaamini Roho Mtakatifu anahuisha, anathibitisha wokovu, anahukumu dhambi, anatuongoza katika kweli yote, na anatujulisha Kristo katika maisha ya kanisa (Yn. 14:16–17, 26; Yn. 16:13–14). Hivyo, Roho Mtakatifu si nguvu isiyo na utu, bali ni nafsi halisi ya tatu katika uungu wa Mungu Mmoja.

Tunaamini mafundisho ya Utatu yanaonekana wazi katika Maandiko, ingawa neno “Utatu” lenyewe halipo moja kwa moja katika Biblia. Tunaona ufunuo huu katika agizo la ubatizo, ambapo Yesu aliamuru wanafunzi kubatiza “kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu” (Mathayo 28:19). Tunaona pia baraka ya mitume ikitaja nafsi zote tatu kwa usawa wa kiungu, “Neema ya Bwana Yesu Kristo, na pendo la Mungu, na ushirika wa Roho Mtakatifu, na iwe pamoja nanyi nyote” (2 Wakorintho 13:14).

Tunaamini wokovu wetu unategemea kikamilifu kazi ya Utatu. Baba alipanga wokovu katika mapenzi yake ya milele, Mwana alitimiza wokovu kwa kifo na ufufuo wake, na Roho Mtakatifu anautumia wokovu huo katika maisha ya waamini kwa kuleta toba, imani, na maisha mapya. Kwa hiyo, hatumwabudu Mungu kwa mgawanyiko, bali tunamwabudu Mungu mmoja aliye hai, akitenda kazi kwa ukamilifu katika nafsi tatu.

Tunaamini maisha ya Kikristo hayawezi kueleweka bila Utatu. Maombi yetu yanaelekezwa kwa Baba, kwa jina la Mwana, katika uwezo wa Roho Mtakatifu. Ibada yetu ni mwitikio kwa kazi ya Mungu aliyejifunua kama Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Ushirika wetu kama kanisa unaakisi umoja ndani ya Utatu, ambapo kuna tofauti ya nafsi lakini umoja wa upendo na kusudi.

Kwa hiyo, kama kanisa, tunashikilia mafundisho ya Utatu kwa unyenyekevu na heshima, tukitambua kuwa ni fumbo linalozidi akili ya mwanadamu, lakini pia ni ukweli uliofunuliwa wazi katika Maandiko. Tunakiri Utatu si hoja ya kitaaluma tu, bali ni msingi wa imani yetu, ibada yetu, na tumaini letu la wokovu. Tunamwabudu Mungu mmoja, Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu, sasa na hata milele.

3. Kuhusu Mwanadamu na Dhambi

Tunaamini mwanadamu aliumbwa na Mungu kwa kusudi maalumu, kwa mfano na sura ya Mungu, ili aishi katika uhusiano wa upendo, utiifu, na utukufu wa Mungu. Uumbaji wa mwanadamu haukuwa ajali wala matokeo ya nguvu zisizo na mpango, bali ulikuwa tendo la makusudi la Mungu mwenye hekima na mapenzi. Maandiko yanasema wazi, “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu” (Mwanzo 1:26). Hii ina maana kwamba mwanadamu alipewa heshima ya kipekee, uwezo wa kiroho, maadili, na wajibu wa kuitunza na kuitawala dunia chini ya mamlaka ya Mungu.

Tunaamini mwanadamu aliumbwa mwema, mtakatifu, na asiye na hatia, lakini alipewa pia hiari ya kuchagua. Kupitia uasi wa Adamu na Hawa, dhambi iliingia duniani, na kwa dhambi hiyo uhusiano kati ya Mungu na mwanadamu ukavunjika. Maandiko yanatufundisha kuwa “kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti ikaingia” (Warumi 5:12). Dhambi haikuwa kosa dogo la kimaadili, bali ilikuwa uasi wa wazi dhidi ya amri ya Mungu, ulioleta matokeo makubwa kwa vizazi vyote vya wanadamu.

Tunaamini dhambi iliathiri mwanadamu mzima. Akili ilipotoshwa, mapenzi yakapindishwa, hisia zikachafuliwa, na mahusiano yakaharibika. Hali hii ya upotovu haimaanishi kwamba mwanadamu amepoteza kabisa sura ya Mungu, bali sura hiyo imeharibiwa na kuchafuliwa na dhambi. Kwa hiyo, hata matendo mema ya mwanadamu hayawezi kumrejesha katika haki kamili mbele za Mungu. Kama Maandiko yanavyosema, “hakuna mwenye haki hata mmoja” (Warumi 3:10), na “wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu” (Warumi 3:23).

Kanisa la kwanza lilitambua mapema uzito wa fundisho hili, hasa katika kukabiliana na mafundisho yaliyodharau athari ya dhambi na kudai kuwa mwanadamu anaweza kuokoka kwa juhudi zake mwenyewe. Mababa wa kanisa walisisitiza kuwa dhambi ya asili ni hali ya ndani inayomfanya mwanadamu awe mtumwa wa dhambi, na hivyo kumhitaji Mungu achukue hatua ya kwanza katika wokovu. Hii ililindwa baadaye katika mafundisho ya Mageuzi ya kanisa, yaliyosisitiza kwamba mwanadamu hawezi kujikomboa mwenyewe bila neema ya Mungu.

Tunaamini matokeo ya dhambi ni mauti ya kiroho na ya kimwili, hukumu ya haki ya Mungu, na kutengwa na Mungu. Maandiko yanatuonya wazi kwamba “mshahara wa dhambi ni mauti” (Warumi 6:23). Hii inahusu si kifo cha mwili tu, bali pia hali ya kutengwa na Mungu, sasa na milele, kama dhambi haitatubiwa. Hivyo, tatizo la mwanadamu si mazingira tu, elimu, au mfumo wa kijamii, bali ni moyo wake uliopotoka unaohitaji kubadilishwa.

Tunaamini hata katika hali hii ya dhambi, Mungu hakumwacha mwanadamu bila tumaini. Mara baada ya kuanguka, Mungu alitoa ahadi ya ukombozi, akionesha kuwa uzao wa mwanamke angeshinda nguvu za uovu (Mwanzo 3:15). Hii inaonesha kwamba wokovu haukuwa wazo la baadaye, bali ulikuwa sehemu ya mpango wa Mungu tangu mwanzo. Hivyo, ufahamu sahihi wa dhambi hutuweka tayari kuelewa uzuri na uzito wa neema ya Mungu katika Kristo.

Tunaamini ufahamu wa kweli wa dhambi hutuletea unyenyekevu, toba, na utegemezi wa Mungu. Kanisa halijaitwa kuficha dhambi wala kuipunguza uzito wake, bali kuitangaza kwa uaminifu ili Injili ionekane kuwa habari njema kweli. Bila kuelewa dhambi, hatuwezi kuelewa msalaba; kama ilivyo katika ugonjwa; bila kutambua ugonjwa, hatuwezi kuthamini tiba. Kwa hiyo, tunafundisha kwa uaminifu hali ya mwanadamu katika dhambi, ili watu wamtumainie Kristo kwa wokovu kamili na maisha mapya.

4. Kuhusu Wokovu

Tunaamini wokovu ni kazi ya Mungu kwa neema yake, uliopangwa tangu milele, uliofunuliwa katika historia, na unaotimizwa kikamilifu katika Yesu Kristo. Wokovu hauanzi na jitihada za mwanadamu, bali huanza na mapenzi ya Mungu mwenye rehema, anayemtafuta mwenye dhambi ili amrejeshe kwake. Maandiko yanathibitisha wazi kwamba “wote wamefanya dhambi” na hawawezi kujipatia haki mbele za Mungu kwa matendo yao wenyewe, hivyo wokovu ni zawadi ya neema, si thawabu ya juhudi (Warumi 3:23, Waefeso 2:8–9).

Tunaamini Yesu Kristo ndiye msingi na kiini cha wokovu wetu. Yeye ni Mwana wa Mungu aliyefanyika mwili, akaishi maisha kamilifu yasiyo na dhambi, akatimiza sheria kikamilifu, kisha akajitoa mwenyewe msalabani kama dhabihu ya upatanisho kwa ajili ya dhambi zetu. Maandiko yanasema, “Lakini Mungu aonesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu tulipokuwa tungali wenye dhambi” (Warumi 5:8). Kifo cha Kristo hakikuwa ajali ya kihistoria, bali kilikuwa kitendo cha makusudi cha upendo na haki ya Mungu kukutana pamoja.

Tunaamini wokovu hupokelewa kwa njia ya toba na imani. Toba ni mgeuko wa ndani unaoongozwa na Roho Mtakatifu, unaomhusisha mtu kuiacha dhambi na kumgeukia Mungu kwa unyenyekevu. Imani ni kumtumainia Kristo kikamilifu, si tu kwa maneno, bali kwa moyo na maisha. Yesu mwenyewe alisema, “Tubuni, mkaamini Injili” (Marko 1:15). Hivyo, toba na imani haviwezi kutenganishwa, kwa kuwa imani ya kweli huzaa toba ya kweli.

Tunaamini wakati mtu anapomwamini Kristo kwa kweli, Mungu humhesabia haki kwa neema, si kwa matendo. Hii ndiyo haki ya kuhesabiwa, ambapo mwenye dhambi hutangazwa kuwa mwenye haki mbele za Mungu kwa sababu ya haki ya Kristo, si kwa sababu ya haki yake mwenyewe. Paulo anasema, “Tukihesabiwa haki kwa imani, tuna amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo” (Warumi 5:1). Hii ni msingi wa uhakika wa wokovu wetu, kwa kuwa unategemea kazi ya Kristo, si uthabiti wa hisia zetu.

Tunaamini wokovu hauishii katika kusamehewa dhambi tu, bali huleta maisha mapya. Yule aliyeokolewa huanza safari ya utakaso, ambapo Roho Mtakatifu humbadilisha hatua kwa hatua ili afanane na Kristo. Hii ni kazi endelevu ya neema, inayoonekana katika matunda ya Roho, upendo wa haki, na chuki dhidi ya dhambi. Kama Maandiko yanavyosema, “hata imekuwa mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya” (2 Wakorintho 5:17).

Tunaamini wokovu wa kweli huzaa uvumilivu katika imani. Mungu anayemwokoa mtu, humlinda na kumaliza kazi njema aliyoianza ndani yake. Hii haitoi ruhusa ya kuishi katika dhambi, bali huleta moyo wa shukrani na utiifu. Yesu alisema, “kondoo wangu huisikia sauti yangu, nami nawajua, nao wanifuata” (Yohana 10:27–28). Hivyo, wokovu huonekana kwa kuendelea kumfuata Kristo kwa uaminifu.

Tunatangaza Injili ya neema kwa ujasiri na upendo, tukiwaita watu wamgeukie Kristo kwa toba na imani. Tunakataa Injili inayompunguzia Kristo kazi yake au inayomweka mwanadamu katikati ya wokovu wake mwenyewe. Tunashikilia kwa furaha kwamba wokovu ni wa Bwana, umetolewa kwa neema, na umepatikana kwa imani, kwa lengo la kumtukuza Mungu.

Kwa hiyo, kazi ya wokovu ni kazi ya Mungu kuanzia mwanzo hadi mwisho, kwa maana yeye ndiye aliyepanga kusudi la ukombozi, alimtuma Mwana, na anatenda kazi kupitia Roho Mtakatifu katika mioyo ya watu; na mwanadamu hana mchango wowote katika kuanzisha, kulipia, wala kukamilisha wokovu huo, isipokuwa kuupokea kwa imani na kuitikia kwa toba ya kweli. Wokovu hauzaliwi na mapenzi ya mwili wala juhudi za kibinadamu, bali unatokana na neema ya Mungu inayotutangulia, inayotuvuta, na inayotuhifadhi, ili utukufu wote urudi kwake yeye peke yake.

5. Kuhusu Kanisa

Tunaamini kanisa ni mwili wa Kristo duniani, ulioundwa na wote waliomwamini Yesu Kristo kwa toba na imani ya kweli. Kanisa si jengo, si dhehebu, wala si taasisi ya kibinadamu tu, bali ni watu wa Mungu walioitwa kutoka gizani kuingia katika nuru yake ya ajabu. Maandiko yanasema wazi kwamba Kristo “ndiye kichwa cha mwili, yaani kanisa” (Wakolosai 1:18). Hivyo, uhai, mwelekeo, na mamlaka ya kanisa hutoka kwa Kristo mwenyewe.

Tunaamini kanisa linaonekana katika sura mbili. Kwanza ni kanisa la ulimwengu mzima, ambalo linajumuisha waamini wote wa kweli wa nyakati zote na mahali pote, waliounganishwa na Kristo kwa Roho mmoja. Pili ni kanisa la mahali, ambapo waamini hukusanyika kwa utaratibu katika eneo fulani kwa ajili ya ibada, mafundisho, ushirika, maombi, na huduma. Maandiko yanatuonesha wazi mfano huu katika kanisa la kwanza, “wakadumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kumega mkate, na katika kusali” (Matendo 2:42).

Tunaamini kanisa la mahali si jambo la hiari kwa Mkristo, bali ni sehemu ya utiifu na uanafunzi. Mtu aliyeokolewa huunganishwa na Kristo, na kwa hiyo huunganishwa pia na mwili wake. Hakuna Ukristo wa peke yako unaopatana na Maandiko. Kanisa ndilo mahali ambapo waamini hulindwa, hufundishwa, husahihishwa, na kujengwa katika imani. Ndani ya kanisa, Mungu ametupa zawadi ya ushirika ili tubebeane mizigo na kukua pamoja katika upendo na ukweli.

Tunaamini kanisa limeitwa kufanya kazi kuu nne. Kwanza ni kumwabudu Mungu kwa moyo na kweli, kwa maneno na kwa maisha. Pili ni kufundisha Neno la Mungu kwa uaminifu, ili watakatifu wakue katika maarifa na utiifu. Tatu ni kushuhudia Injili kwa maneno na matendo, ili ulimwengu umjue Kristo. Nne ni kuwajenga waamini kupitia ufuasi, huduma, na nidhamu ya kiroho. Maandiko yanasema Kristo alitoa vipawa ndani ya kanisa “ili kuwakamilisha watakatifu hata kazi ya huduma itimizwe, hata mwili wa Kristo ujengwe” (Waefeso 4:12).

Tunaamini Kristo ndiye kichwa pekee cha kanisa, na mamlaka yote ya kanisa yapo chini yake. Uongozi wa kanisa ni huduma, si nafasi ya kutawala kwa mabavu. Viongozi wa kiroho wameitwa kulilinda kundi, kulifundisha, na kulitumikia kwa unyenyekevu na mfano mwema. Kama Maandiko yanavyosema, wachungaji wanapaswa kulichunga kundi la Mungu “si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari; wala si kwa kutafuta faida ya aibu, bali kwa moyo wa kupenda” (1 Petro 5:2).

Tunaamini kanisa pia limeitwa kudumisha nidhamu ya kiroho kwa upendo na hekima. Nidhamu si adhabu ya kikatili, bali ni tendo la upendo linalolenga kurejesha, kulinda utakatifu wa kanisa, na kumtukuza Kristo. Yesu mwenyewe alifundisha kuhusu kurekebishana kwa upendo ndani ya jumuiya ya waamini, ili dhambi isiachwe iendelee bila kushughulikiwa (Mathayo 18:15).

Tunaamini kanisa ni familia ya kiroho. Ndani yake kuna utofauti wa karama, vipawa, na majukumu, lakini kuna umoja mmoja katika Kristo. Hakuna mshirika asiye na umuhimu, wala hakuna aliye juu kuliko wengine katika thamani mbele za Mungu. Kama Paulo anavyofundisha, “mwili ni mmoja, nao una viungo vingi” na kila kiungo kina kazi yake (1 Wakorintho 12:12). Umoja huu unatuhimiza kuheshimiana, kushirikiana, na kutumikiana kwa upendo.

Kwa hiyo, kama kanisa, tunakiri kwa unyenyekevu na furaha kwamba tumeitwa kuwa mwili wa Kristo duniani. Tunajitahidi kuishi chini ya uongozi wake, tukisimama katika kweli ya Neno, tukijengwa katika upendo, na tukitimiza utume wake hadi atakaporudi.

6. Kuhusu Malaika

Tunaamini malaika ni viumbe wa kiroho walioumbwa na Mungu, si wa milele kama Mungu, bali wako chini ya mamlaka yake na hutenda mapenzi yake. Maandiko yanaonesha wazi kwamba malaika waliumbwa na Mungu kwa kusudi la kumtukuza, kumwabudu, na kutekeleza maagizo yake katika historia ya wokovu. Kama Zaburi inavyosema, “Mhimidini BWANA, enyi malaika zake, Ninyi mlio hodari, mtendao neno lake, Mkiisikiliza sauti ya neno lake.” (Zaburi 103:20). Hivyo, malaika si kitu cha kuabudiwa, bali ni watumishi wa Mungu aliye hai.

Tunaamini Maandiko yanatufundisha uwepo wa makundi mawili makuu ya malaika. Kundi la kwanza ni malaika walio safi, waliobaki katika utiifu kwa Mungu, na kundi la pili ni malaika waasi, walioanguka pamoja na Shetani. Tofauti hii ni muhimu ili kanisa liwe na ufahamu wa kibiblia usiochanganya ukweli na uvumi wa kiroho.

Tunaamini malaika walio safi ni watakatifu katika utumishi wao, wakikaa katika uwepo wa Mungu, wakimsifu, na kutumwa kutekeleza mapenzi yake. Maandiko yanawaeleza malaika hawa kama “Je! Hao wote si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu?” (Waebrania 1:14). Hii inaonesha kwamba Mungu, kwa rehema yake, hutumia malaika kama vyombo vya ulinzi, uongozi, na msaada kwa watu wake, ingawa hatujaambiwa majina wala idadi yao kwa kina.

Tunaamini Biblia inataja aina na majina fulani ya malaika kwa kusudi maalumu. Mikaeli anaelezwa kama malaika mkuu, mwenye jukumu la kipekee katika vita vya kiroho na ulinzi wa watu wa Mungu (Danieli 10:13, 21; Yuda 1:9). Gabrieli anaonekana kama mjumbe wa Mungu, akileta ujumbe wa ufunuo, hasa kuhusu mpango wa wokovu (Danieli 8:16; Luka 1:19, 26). Pia Maandiko yanataja makerubi na maserafi, malaika wanaohusishwa na utukufu, utakatifu, na ibada mbele za Mungu (Isaya 6:2–3; Mwanzo 3:24). Haya yote yanatuonesha kuwa malaika wana majukumu tofauti, lakini wote wako chini ya amri ya Mungu mmoja.

Tunaamini kwamba katika ibada ya kweli, kanisa la duniani linaunganishwa kiroho na kanisa la mbinguni, na hivyo malaika watakatifu wanaweza kushiriki pamoja nasi katika kumwabudu Mungu, si kama wanaoabudiwa wala kuwa kitovu cha ibada, bali kama roho watumikao waliotumwa kuhudumia wale watakaourithi wokovu kama inavyosema Waebrania 1:14, na kwamba tunapomkaribia Mungu katika Kristo tunaifikilia Yerusalemu wa mbinguni na majeshi ya malaika elfu nyingi kama ilivyoandikwa katika Waebrania 12:22, kwa hiyo ibada yetu ni tukio la kiroho linaloshirikisha mbingu na nchi chini ya ukuu wa Kristo peke yake.

Tunaamini pia yapo majeshi ya malaika waasi, yaliyoongozwa na Shetani. Shetani alikuwa malaika aliyeasi kwa kiburi na kutaka kujitukuza, na akaanguka pamoja na malaika waliomfuata. Yesu mwenyewe alisema, “Nalimwona Shetani akianguka kutoka mbinguni kama umeme” (Luka 10:18). Malaika hawa waasi wanajulikana pia kama pepo au roho wachafu, nao wanapinga kazi ya Mungu, wakidanganya, wakipotosha, na kujaribu kuharibu kazi ya Injili.

Tunaamini Shetani si sawa na Mungu, wala si nguvu inayolingana na Mungu. Yeye ni kiumbe aliyeumbwa, aliyeasi, na mwenye mwisho uliokwishaamuliwa. Maandiko yanaonesha wazi kwamba mamlaka ya Shetani ni finyu na iko chini ya ruhusa ya Mungu. Kupitia msalaba, Kristo aliwashinda waziwazi falme na mamlaka za giza. “akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.” (Wakolosai 2:15). Hivyo, ushindi wa mwisho si wa Shetani, bali ni wa Kristo.

Tunaamini waamini wameitwa kuishi kwa ufahamu wa vita vya kiroho, lakini bila hofu. Hatuitwi kuzungumza na malaika, kuwaabudu, wala kuwatafuta kwa njia za siri. Tunaitwa kumtii Mungu, kusimama katika kweli ya Neno, na kuvaa silaha za kiroho alizotupa Mungu. Kama Maandiko yanavyosema, “jivikeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kusimama juu ya hila za Shetani” (Waefeso 6:11).

Tunaamini mamlaka ya kanisa na ya muumini iko katika Kristo pekee. Kwa jina lake, kwa damu yake, na kwa Neno lake, nguvu za giza hushindwa. Malaika walio safi hutenda mapenzi ya Mungu, malaika waasi hutetemeka mbele ya mamlaka ya Kristo, na kanisa linaishi kwa ushindi si kwa nguvu zake, bali kwa neema ya Mungu.

Kwa hiyo, kama kanisa, tunakiri kwa uwiano na unyenyekevu fundisho la malaika kama linavyofundishwa katika Maandiko. Tunamheshimu Mungu aliyeumba malaika, tunamtukuza Kristo aliyewashinda maadui wote, na tunatembea katika nuru, tukijua kwamba “yeye aliye ndani yetu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia” (1 Yohana 4:4).

7. Kuhusu Ndoa na Familia

Tunaamini kwamba ndoa halali ni muungano wa agano kati ya mwanamume na mwanamke uliowekwa na Mungu tangu mwanzo wa uumbaji, (Mwanzo 2:24), na kwamba muungano huo si makubaliano ya muda bali ni agano la kudumu linalounganisha mwili, nafsi na roho; tunaamini pia kuwa ndoa hiyo inapaswa kuthibitishwa na mashahidi watatu wanaowakilisha nyanja kuu za maisha ya mwanadamu; kwanza, wazazi au walezi na jamii kama uthibitisho wa kijamii na kihistoria unaolinda heshima na uwajibikaji wa kifamilia, pili, serikali kama mamlaka iliyowekwa na Mungu kwa ajili ya utaratibu na ulinzi wa haki za kiraia (Warumi 13:1) na tatu, kanisa kama shahidi wa kiroho linalosimama mbele za Mungu kuthibitisha agano hilo, kwa kuwa ndoa ni fumbo linaloakisi uhusiano wa Kristo na Kanisa kama (Waefeso 5:31-32). Hivyo tunaona kwamba uthibitisho huu wa kijamii, kisheria na kiroho unaifanya ndoa kuwa taasisi kamili inayotambulika mbele za Mungu na wanadamu, na kwa kanuni ya Kumbukumbu la Torati 19:15 kwamba neno huthibitika kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu, tunaweka msimamo kwamba ndoa halali ni ile inayosimama katika ushuhuda huo kamili.

Tunaamini kwamba watoto ni zawadi na urithi kutoka kwa Bwana, si matokeo ya juhudi za kibinadamu pekee bali ni neema yake juu ya familia, kama Maandiko yanavyothibitisha kwamba watoto ni urithi wa Bwana na uzao ni thawabu (Zaburi 127:3), na kwamba uzao mwema ni baraka inayotoka kwake (Zaburi 128:3); hata hivyo tunaamini pia kwamba kukosekana kwa watoto ndani ya ndoa si laana wala hukumu ya Mungu, kwa maana katika historia ya wokovu tunaona mifano ya watu waadilifu waliokaa muda mrefu bila watoto na bado walikuwa katika mpango mkamilifu wa Mungu, kama vile Ibrahimu na Sara (Mwanzo 11:30; 21:1-2), Hana (1 Samweli 1:5-6), na Zakaria na Elizabeti ambao waliitwa wenye haki mbele za Mungu hata kabla ya kupata mtoto (Luka 1:6-7); kwa hiyo thamani ya ndoa haipimwi kwa uwezo wa kuzaa bali kwa uaminifu wa agano na upendo wa wanandoa, kwa kuwa kila jambo lina wakati wake uliowekwa na Mungu (Mhubiri 3:1), na mpango wake juu ya maisha ya wanadamu hubaki kuwa mwema hata pale ambapo matarajio ya kibinadamu hayajatimia (Yeremia 29:11).

Tunaamini kwamba malezi ya watoto ni wito mtakatifu na jukumu la moja kwa moja kutoka kwa Mungu kwa wazazi, kwa kuwa watoto ni urithi wake na wanakabidhiwa katika mikono ya familia ili wafundishwe njia za Bwana tangu wakiwa wadogo (Zaburi 127:3; Mithali 22:6); tunaamini kwamba malezi si jukumu la shule au kanisa pekee bali ni agizo la agano lililotolewa wazi kwa wazazi kufundisha kwa bidii, kwa maneno na kwa matendo, katika maisha ya kila siku (Kumbukumbu la Torati 6:6-7), na kwamba nidhamu ya upendo ni sehemu ya malezi ya kimungu, si kwa ukali wa hasira bali kwa kusudi la kujenga tabia na hekima (Mithali 13:24; Waefeso 6:4); tunaamini pia kwamba lengo la malezi si tu mafanikio ya kidunia bali kumlea mtoto katika kumcha Mungu na kumjua Kristo, kwa kuwa mwanzo wa hekima ni kumcha Bwana (Mithali 9:10), na kwamba wazazi watawajibika mbele za Mungu kwa namna walivyolilea kizazi walichokabidhiwa (Kumbukumbu la Torati 4:9).

8. Kuhusu Mambo ya Mwisho

Tunaamini historia yote inaelekea katika utimilifu wa mpango wa Mungu, na mwisho wa mambo yote uko mikononi mwa Mungu mwenyewe. Mambo ya mwisho si hadithi za kuogopesha waamini wala ramani za kubahatisha tarehe, bali ni ufunuo wa tumaini, haki, na ushindi wa Kristo. Maandiko yanatufundisha kwamba Mungu anatawala sasa, ametawala tangu mwanzo, na ataendelea kutawala hadi mwisho.

Tunaamini Yesu Kristo tayari ni Mfalme anayeketi katika mamlaka, baada ya kufufuka na kupaa kwake mbinguni. Ufalme wa Mungu haujaahirishwa hadi wakati wa baadaye, bali tayari umeanza kwa kuja kwa Kristo, unaendelea sasa katika mioyo ya waamini na maisha ya kanisa, na utatimia kikamilifu atakaporudi tena katika utukufu wake. Kama Yesu mwenyewe alivyosema, “ufalme wa Mungu umo ndani yenu” (Luka 17:21). Hii inatufundisha kwamba sasa tunaishi katika kipindi cha kati, ambapo Kristo anatawala, na kanisa linaishi kati ya ahadi ya utimilifu wake wa mwisho.

Tunaamini kipindi cha sasa ni wakati ambao Injili inahubiriwa kwa mataifa yote, kanisa linajengwa, na mapambano kati ya nuru na giza yanaendelea. Uovu bado upo, mateso yapo, na majaribu yapo, lakini mamlaka ya mwisho tayari ni ya Kristo. Shetani Alishashindwa, ingawa bado anafanya kazi kwa muda mfupi uliobaki. Maandiko yanaonesha hali hii ya mvutano kwa kusema kwamba Kristo “sharti atawale hata awaweke adui zake wote chini ya miguu yake” (1 Wakorintho 15:25).

Tunaamini Biblia haitufundishi ufalme wa Kristo wa muda maalumu wa kidunia kabla ya mwisho wa historia, bali inatufundisha utawala wa Kristo wa sasa unaoelekea kwenye mwisho wa ghafla na wa hakika. Kurudi kwa Kristo hakutakuwa kwa awamu nyingi, bali kutakuwa tukio moja kuu, la wazi, na la utukufu, litakaloshuhudiwa na wote. Maandiko yanasema, “tazama, anakuja na mawingu, na kila jicho litamwona” (Ufunuo 1:7). Hivyo, kanisa haliitwi kusubiri enzi ya kidunia ya baadaye, bali kuishi kwa uaminifu sasa.

Tunaamini wakati Kristo atakaporudi, kutakuwa na ufufuo wa wafu wote; wenye haki na wasio haki. Wale walio ndani ya Kristo watafufuliwa kwa ajili ya uzima wa milele, na wale wasiomwamini watafufuliwa kwa ajili ya  hukumu ya milele. Yesu mwenyewe alisema wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake, nao watatoka (Yohana 5:28–29). Huu utakuwa mwisho wa historia ya sasa na mwanzo wa hali ya milele.

Tunaamini kutakuwa na hukumu ya mwisho, ambapo Mungu atahukumu ulimwengu kwa haki kwa njia ya Yesu Kristo. Hukumu hii itakuwa ya haki kamili, bila upendeleo, na itadhihirisha haki ya Mungu na ukweli wa mioyo ya wanadamu. Kwa waamini, hukumu hii haitakuwa hukumu ya adhabu, kwa kuwa adhabu yao ilichukuliwa na Kristo msalabani. Kwa wasio waamini, hukumu itakuwa udhihirisho wa haki ya Mungu dhidi ya dhambi isiyotubiwa. Maandiko yanasema, “Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu” (Waebrania 9:27).

Tunaamini mwisho wa mambo yote si uharibifu tu, bali ni uumbaji mpya. Mungu ataumba mbingu mpya na nchi mpya, ambamo haki itakaa, na mateso, machozi, mauti, na dhambi havitakuwepo tena. Ufunuo unatupa tumaini hili kwa maneno haya, “Nikaona mbingu mpya na nchi mpya… Mungu atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena” (Ufunuo 21:1–4). Hili ndilo tumaini kuu la kanisa, si kuokoka kutoka duniani tu, bali kurejeshwa kwa uumbaji wote chini ya utawala wa Mungu.

Tunaamini mafundisho ya mambo ya mwisho yanapaswa kutufanya tuishi maisha ya utakatifu, uaminifu, na bidii katika kazi ya Bwana. Tumaini la kurudi kwa Kristo halitufanyi tukimbie dunia, bali hutufanya tuishi kwa makusudi zaidi ndani yake. Kama mtume Petro anavyouliza, “Basi, kwa kuwa vitu hivi vyote vitafumuliwa hivyo, imewapasa ninyi kuwa watu wa tabia gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa,” 2 Pet 3:11

Kwa hiyo, kama kanisa, tunaishi tukitazama mbele kwa matumaini, tukimtumikia Mungu kwa uaminifu sasa, na tukingojea kwa subira kurudi kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Hatuhubiri hofu, bali tumaini. Hatufundishi kubahatisha nyakati, bali kuishi katika nuru. Tunakiri kwamba Kristo anatawala sasa, Kristo atarudi tena, na Kristo atafanya vitu vyote kuwa vipya, kwa utukufu wa Mungu na furaha ya watu wake.

Tunaamini kwamba Mwamini anapokufa, anaungana moja kwa moja na Kristo katika utukufu wake (Wafilipi 1:23, 2 Wakorintho 5:8); hivyo roho ya mwenye haki huingia mara moja katika uwepo wa Bwana akingojea ufufuo wa mwili siku ya mwisho; na kwamba mtu asiyeamini anapokufa anaungana moja kwa moja na hali ya hukumu na maumivu akingojea hukumu ya mwisho, kama Bwana Yesu alivyoeleza katika Luka 16:23. Kwa hiyo tunashikilia kuwa kuna hali ya fahamu mara baada ya kifo, tofauti kati ya wenye haki na wasioamini, yote chini ya haki na mamlaka ya Mungu.

B. KUHUSU MAZOEZI

1. Ibada za Pamoja za Kanisa

Tunaamini kwamba siku ya Jumapili ndiyo siku ya kumwabudu Mungu kwa kukusanyika pamoja kama kanisa, na ndiyo Sabato ya Kikristo, kwa kuwa ni siku ambayo Bwana wetu Yesu Kristo alifufuka katika wafu kama ilivyoandikwa katika Mathayo 28:1, na siku hiyo hiyo wanafunzi walikusanyika kama inavyoshuhudiwa katika Yohana 20:19, na tena kanisa la kwanza lilikuwa likikusanyika siku ya kwanza ya juma kwa kuumega mkate na kusikiliza Neno kama ilivyoandikwa katika Matendo 20:7, na mtume Paulo aliagiza matoleo yatengwe siku ya kwanza ya juma kama ilivyoandikwa katika 1 Wakorintho 16:2, hivyo kwa msingi wa ufufuo wa Kristo na ushuhuda wa kanisa la mitume, tunaona kuwa Jumapili, Siku ya Bwana, ndiyo siku ya ibada ya kikristo, si kwa kuirudia sheria ya torati kama ilivyokuwa chini ya agano la kale, bali kwa kuadhimisha ukombozi uliokamilishwa katika Kristo na kuingia katika pumziko lake la neema kama inavyofundishwa katika Waebrania 4:9-10.

Tunaamini ibada za pamoja za kanisa ni mwitikio wa watu wa Mungu kwa ufunuo wa Mungu mwenyewe. Ibada haianzi na matakwa ya wanadamu, mitindo, au hisia, bali huanza na Mungu anayejifunua kupitia Neno lake na kazi yake ya wokovu. Kwa hiyo, ibada ni tendo la kiroho ambapo kanisa hukusanyika kwa kusudi la kumtukuza Mungu, kumsikiliza, na kujitoa upya kwake. Maandiko yanatufundisha, “Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli” (Yohana 4:24).

Tunaamini ibada ya pamoja ni ya lazima kwa maisha ya Mkristo, si jambo la ziada. Kanisa la kwanza lilidumisha desturi ya kukusanyika mara kwa mara kwa ajili ya ibada, mafundisho, na maombi. Maandiko yanasema, “wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine” (Waebrania 10:25). Kukusanyika pamoja ni ishara ya utiifu, upendo kwa mwili wa Kristo, na utambuzi kwamba hatuwezi kuishi imani peke yetu.

Tunaamini ibada ya pamoja inapaswa kujengwa juu ya Neno la Mungu. Mahubiri si hotuba za motisha wala maoni ya mtu binafsi, bali ni ufafanuzi na matumizi ya Maandiko. Kupitia kusomwa na kufundishwa kwa Neno, Mungu hunena na watu wake, akiwaita kwenye toba, imani, na utiifu. Kama Paulo anavyomwagiza Timotheo, “lihubiri neno, uwe tayari wakati ufaao na wakati usiofaa” (2 Timotheo 4:2). Hivyo, Neno ndilo kiini cha ibada zetu.

Tunaamini ibada za pamoja zinahusisha pia maombi, sifa, na shukrani. Kupitia nyimbo, zaburi, na tenzi za rohoni, kanisa humkiri Mungu, hutangaza kazi zake, na kujenga imani ya waamini. Maandiko yanasema, “neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu… mkifundishana na kuonyana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni” (Wakolosai 3:16). Muziki katika ibada si burudani, bali ni huduma ya kiroho inayolenga kumtukuza Mungu na kulijenga kanisa.

Tunaamini ibada ya kweli inahitaji mpangilio na heshima. Mungu si Mungu wa machafuko, bali wa amani. Hivyo, hata pale ambapo kanisa linatoa nafasi kwa kazi na karama za Roho Mtakatifu, mambo yote yanapaswa kufanyika kwa adabu, hekima, na kwa lengo la kujenga mwili wa Kristo (1 Wakorintho 14:26, 40). Uhuru wa kiroho haupingani na nidhamu, bali huenda pamoja.

Tunaamini ibada za pamoja zinapaswa kuathiri maisha ya waamini nje ya ukumbi wa ibada. Ibada ya kweli hutufanya tumtii Mungu katika kazi, familia, jamii, na huduma. Kama Maandiko yanavyosema, “itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana” (Warumi 12:1).

Kwa hiyo, kama kanisa, tunajitahidi kudumisha ibada za pamoja zilizojaa heshima ya Mungu, zinazoongozwa na Neno, zilizo hai kupitia kazi ya Roho Mtakatifu, na zinazoelekeza mioyo ya watu kwa Kristo. Tunakusanyika si kwa desturi tu, bali kwa imani, tukijua kwamba Mungu hukutana na watu wake wanapokusanyika kwa jina lake, na kanisa hujengwa kwa utukufu wake.

2. Maombi ya Pamoja na ya Binafsi

Tunaamini maombi ni sehemu ya msingi ya uhusiano wa waamini na Mungu, na ni njia ambayo Mungu ameichagua ili watu wake washirikiane naye katika mapenzi yake duniani. Maombi si mbinu ya kumlazimisha Mungu atende tunavyotaka, bali ni tendo la unyenyekevu la kumkaribia Mungu, kumtegemea, na kuoanisha mioyo yetu na mapenzi yake. Maandiko yanatufundisha wazi, “Msijisumbue kwa neno lolote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba pamoja na kushukuru haja zenu na zijulikane na Mungu” (Wafilipi 4:6).

Tunaamini Yesu Kristo mwenyewe ndiye mfano wetu mkuu wa maisha ya maombi. Kabla ya kufanya maamuzi muhimu, katika nyakati za shinikizo, na hata katika mateso, Yesu alitenga muda wa kuwa peke yake na Baba kwa maombi. Maandiko yanasema, “naye akaondoka akaenda mahali pasipo na watu, akaomba” (Marko 1:35). Hii inatufundisha kwamba hata huduma iliyojaa nguvu haibadilishi hitaji la maombi, bali hulitegemea zaidi.

Tunaamini maombi ya binafsi ni msingi wa afya ya kiroho ya Mkristo. Ndani ya chumba cha faragha, muumini hujifunza kusikiliza sauti ya Mungu kupitia Neno, kuungama dhambi, kupokea rehema, na kuimarishwa ndani. Yesu alifundisha wazi kwamba maombi ya faraghani yana thamani kubwa mbele za Mungu kuliko maonyesho ya nje. “Wewe, uombapo, ingia chumbani mwako, ukafunge mlango, umwombe Baba yako aliye sirini” (Mathayo 6:6). Maombi ya aina hii hujenga unyenyekevu na uaminifu wa ndani.

Tunaamini maombi ya pamoja ni nguvu ya pekee katika maisha ya kanisa. Wakati waamini wanapokusanyika kuomba kwa umoja, Mungu hutenda kwa namna ya kipekee, akijenga ujasiri, umoja, na ushuhuda wa Injili. Kanisa la kwanza lilikuwa kanisa la maombi, na matokeo yake yalikuwa ni ushindi wa kiroho na upanuzi wa huduma. Maandiko yanasema, “walipokwisha kusali, mahali pale walipokutana pakatikiswa, wote wakajazwa Roho Mtakatifu” (Matendo 4:31). Hii inaonesha uhusiano wa karibu kati ya maombi ya pamoja na kazi ya Roho Mtakatifu.

Tunaamini maombi yanapaswa kuwa ya kudumu, ya dhati, na ya imani. Maombi si ya dharura tu, bali ni mtindo wa maisha. Mtume Paulo aliwahimiza waamini “ombeni bila kukoma” (1 Wathesalonike 5:17), akimaanisha maisha yanayoishi katika hali ya utegemezi wa Mungu kila wakati. Maombi ya imani hayategemei hisia, bali ahadi za Mungu, kwa kujua kwamba Mungu husikia na kujibu kwa hekima yake na kwa wakati wake.

Tunaamini maombi si mbadala wa kazi, bali ni msingi wa kazi. Kuomba hakumaanishi kutofanya chochote, bali ni kufanya kila kitu chini ya uongozi na nguvu za Mungu. Maombi hutufundisha subira, hutupa amani katikati ya magumu, na hutujengea tumaini hata pale majibu yanapochelewa. Kwa waamini, maombi ni ushuhuda wa imani kwamba Mungu yupo, anajali, na anatenda.

Tunaamini kwamba maombi ya kufunga ni nidhamu ya kiroho ambapo mwamini hujinyenyekeza mbele za Mungu kwa kuacha mambo halali kwa muda ili kutafuta uso wake wa Bwana kwa uongozi. Katika Biblia tunaona aina mbalimbali za mifungo kama kuacha kula chakula kwa muda fulani (Esta 4:16), au kuacha vyakula fulani na kujizuia anasa (Daniel 1:8 na 10:2-3), au hata kujizuia mambo fulani halali kwa muda kwa ajili ya kujitoa katika maombi (1 Wakorintho 7:5); hivyo kufunga humsaidia mwamini kuutiisha mwili, kuimarisha maisha ya maombi na nidhamu, kuongeza usikivu kwa sauti ya Mungu na kufanya yasiyowezekana yawezekane (Mathayo 17:21), si kama njia ya kumlazimisha Mungu, bali kama tendo la neema linalomweka mtu karibu zaidi na mapenzi ya Mungu kwa unyenyekevu na imani.

Kwa hiyo, kama kanisa, tunajitolea kudumisha maisha ya maombi ya binafsi na ya pamoja. Tunawahimiza washirika kuwa na nidhamu ya maombi ya kila siku, kushiriki kwa uaminifu katika mikutano ya maombi ya kanisa, na kuishi maisha yanayoongozwa na maombi. Tunaamini kupitia maombi, kanisa hupokea mwelekeo, nguvu, na neema ya kutimiza wito wake katika kizazi chake.

3. Vikundi Vidogo na Ibada za Majumbani

Tunaamini vikundi vidogo na ibada za majumbani ni sehemu muhimu ya maisha ya kanisa, zinazosaidia ufuasi wa karibu, malezi ya kiroho, na ujenzi wa mahusiano ya kweli kati ya waamini. Ingawa ibada za pamoja za kanisa huleta umoja mkubwa, vikundi vidogo hutoa nafasi ya kukua kwa kina, kushirikiana kwa uwazi, na kushiriki maisha ya imani katika mazingira ya karibu na wengine. Mfano huu unaonekana wazi katika kanisa la kwanza, ambapo waamini “walikuwa wakikaa katika hekalu kila siku, na katika nyumba wakivunja mkate” (Matendo 2:46).

Tunaamini vikundi vidogo vina mizizi ya kibiblia na kihistoria. Katika Agano la Kale, Mungu aliwahudumia watu wake kupitia familia na makusanyiko madogo ya kijamii. Yesu mwenyewe alifanya huduma kwa kundi dogo la wanafunzi, akiwafundisha, kuwaombea, na kuwaandaa kwa huduma. Mtume Paulo pia alitumia nyumba kama vituo vya ibada, mafundisho, na ushirika wa waamini (Warumi 16:5; Wakolosai 4:15). Hii inaonesha kwamba ibada za majumbani si mpango wa kisasa tu, bali ni sehemu ya urithi wa kanisa.

Tunaamini vikundi vidogo ni mahali pa Neno la Mungu kusomwa na kutumika kwa vitendo. Ndani ya kundi dogo, waamini wana nafasi ya kuuliza maswali, kushirikiana mafundisho, na kusaidiana kuishi kile wanachojifunza. Hapa, Neno halibaki kuwa maarifa ya kichwani tu, bali hugeuka kuwa maisha yanayoonekana katika tabia, maamuzi, na mahusiano. Kama Maandiko yanavyosema, “tukaangaliane sisi kwa sisi na kuhimizana katika upendo na kazi nzuri;” (Waebrania 10:24).

Tunaamini vikundi vidogo ni mazingira ya maombi ya pamoja, faraja, na kubebeana mizigo. Ndani ya mazingira haya, waamini hujifunza kushiriki furaha na huzuni, kushirikiana katika shida, na kuombeana kwa dhati. Maandiko yanatufundisha, “chukulianeni mizigo, na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo” (Wagalatia 6:2). Hii huimarisha mshikamano wa kiroho na kujenga kanisa kuwa familia halisi.

Tunaamini vikundi vidogo pia ni mahali pa uwajibikaji wa kiroho. Ndani ya kundi dogo, waamini wanaweza kusaidiana kukua katika utakatifu, kukumbushana kweli ya Neno, na kurekebishana kwa upendo pale panapohitajika. Uwajibikaji huu haukusudiwi kudhibiti, bali kulinda na kujenga. Kama Maandiko yanavyosema, “Chuma hunoa chuma; Ndivyo mtu aunoavyo uso wa rafiki yake.” (Mithali 27:17).

Tunaamini vikundi vidogo havipaswi kuchukua nafasi ya ibada ya pamoja ya kanisa, bali vikamilishane nayo. Lengo si kugawanya kanisa, bali kulijenga kwa ngazi tofauti za uhusika na uangalizi wa kiroho. Kila mshirika anahimizwa kushiriki katika kundi dogo kama sehemu ya kujengwa kwake na mchango wake katika mwili wa Kristo.

Kwa hiyo, kama kanisa, tunathamini na kuendeleza vikundi vidogo na ibada za majumbani kama mazingira ya ukuaji wa kina wa kiroho. Tunawahimiza washirika kujitolea katika makundi haya kwa uaminifu, kwa unyenyekevu, na kwa upendo, tukijua kwamba Mungu hutumia mahusiano ya karibu kuwajenga watu wake katika imani, upendo, na utumishi.

4. Sakramenti[1]

Tunaamini sakramenti ni maagizo ya Kristo aliyoyatoa kwa kanisa lake, yanayotumia ishara zinazoonekana ili kueleza, kuthibitisha, na kutangaza neema ya Mungu iliyoahidiwa katika Injili. Kihistoria, neno sakramenti lilitumika na kanisa la mwanzo kuelezea ishara takatifu ambazo Mungu huzitumia kufundisha watu wake. Ni ufafanuzi unaoonekana wa kweli za wokovu zinazohubiriwa kwa maneno.

Tunaamini kwamba sakramenti zilizoamriwa na Bwana wetu Yesu Kristo kwa kanisa lake ni mbili tu, yaani Ubatizo na Meza ya Bwana, kwa kuwa hizi ndizo alizozianzisha wazi katika Agano Jipya, akisema katika Mathayo 28:19, “Basi enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu,” na tena katika 1 Wakorintho 11:23-26 mtume Paulo anaeleza agizo la Bwana kuhusu Meza ya Bwana, “Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu,” hivyo tunaona kwamba sakramenti hizi mbili ni ishara zinazoonekana za neema isiyoonekana, zikiwa zimewekwa na Kristo mwenyewe kama mihuri ya agano jipya, si kama matendo ya kuokoa kwa nguvu zake zenyewe, bali kama vyombo vya neema vinavyothibitisha imani ya mwamini na kumshirikisha katika kazi iliyokamilishwa ya Kristo.

Tunaamini sakramenti haziokoi kwa zenyewe, bali huelekeza kwa Kristo na kazi yake. Thamani ya sakramenti haiko katika maji, mkate, au divai, bali katika ahadi ya Mungu inayothibitishwa kwa imani. Ndiyo maana sakramenti huambatana na Neno, na haziwezi kutenganishwa na imani ya mpokeaji. Kama Agano Jipya linavyofundisha, ishara za nje zinakuwa na maana ya kiroho pale zinapopokelewa kwa imani ya kweli.

Tunaamini ubatizo wa Kikristo ni sakramenti ya kuingia katika jumuiya inayoonekana ya waamini. Kupitia ubatizo, muumini anashuhudia hadharani toba na imani yake kwa Yesu Kristo, na anathibitishwa kuwa ameingizwa katika mwili wa Kristo. Maandiko yanasema, “tulizikwa pamoja naye kwa ubatizo katika mauti, ili kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa utukufu wa Baba, sisi nasi tuenende katika upya wa uzima” (Warumi 6:4). Ubatizo hauondoi dhambi kwa maji, bali unaeleza kwa ishara yale Mungu ameyatenda ndani ya mtu kwa neema.

Tunaamini ubatizo unaunganisha ishara ya nje na ukweli wa ndani. Ni tamko la utiifu kwa amri ya Kristo, na pia ni muhuri wa neema unaomkumbusha muumini kwamba wokovu wake unategemea Kristo pekee.

Tunaamini Meza ya Bwana ni sakramenti ya kudumisha na kulisha imani ya waamini. Kupitia mkate na kikombe, kanisa hukumbuka kifo cha Kristo, hutangaza Injili, na hupokea faraja ya ahadi za Mungu. Yesu mwenyewe alisema, “fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu” (1 Wakorintho 11:24). Meza ya Bwana si kafara mpya, bali ni kumbukumbu hai ya kafara iliyokamilika msalabani.

Tunaamini katika Meza ya Bwana, Kristo yupo kwa namna ya kiroho, si kwa kubadilika kwa vitu, bali kwa imani ya waamini. Sakramenti hii hutualika kujichunguza, kutubu, na kushiriki kwa shukrani, tukitambua umoja wetu kama mwili mmoja wa Kristo. Kama Maandiko yanavyosema, “kwa kuwa mkate ni mmoja, nasi tulio wengi tu mwili mmoja” (1 Wakorintho 10:17).

Kwa hiyo, kama kanisa, tunapokea sakramenti za ubatizo na Meza ya Bwana kwa heshima na furaha. Tunaziona kama zawadi za Mungu kwa kanisa lake, zenye kusudi la kutufundisha, kututia moyo, na kutuimarisha katika imani. Tunashiriki sakramenti si kwa desturi ya kidini, bali kwa imani hai inayomtazama Kristo, chanzo na mkamilishaji wa wokovu wetu.

5. Uinjilisti

Tunaamini uinjilisti ni wito wa msingi wa kanisa, uliotolewa na Bwana Yesu Kristo mwenyewe, wa kutangaza Injili ya wokovu kwa mataifa yote. Uinjilisti si programu ya kanisa tu, bali ni utambulisho wa kanisa. Kanisa lipo kwa ajili ya kumtangaza Kristo kwa wale ambao bado hawajamsikia. Yesu alisema wazi, “mtakuwa mashahidi wangu… hata mwisho wa nchi” (Matendo 1:8).

Tunaamini Injili ndiyo ujumbe wa kipekee ambao kanisa limekabidhiwa. Injili si ushauri wa kimaadili, si falsafa ya maisha, wala si ahadi ya mafanikio ya kidunia, bali ni habari njema kwamba Mungu amemtuma Mwana wake kumwokoa mwenye dhambi kwa neema. Kiini cha uinjilisti ni kutangaza kifo na ufufuo wa Kristo, na kuwaita watu watubu na waamini. Kama Paulo anavyosema, “Injili… ni uwezo wa Mungu uuletayo wokovu kwa kila aaminiye” (Warumi 1:16).

Tunaamini uinjilisti unafanyika kwa maneno na kwa maisha, lakini hauwezi kubadilishwa kuwa matendo pekee bila maneno. Maisha mema ni ushuhuda muhimu wa Injili, lakini maneno ya Injili ni lazima ili watu wamjue Kristo. Kanisa linaitwa kuishi maisha ya upendo, haki, na huruma, lakini pia linaitwa kuzungumza kwa ujasiri na upole kuhusu Kristo na msalaba wake.

Tunaamini Roho Mtakatifu ndiye mwenye kuleta matokeo ya kweli katika uinjilisti. Wajibu wa kanisa ni kupanda na kumwagilia kwa uaminifu, lakini Mungu ndiye anayekuza. Hii inatulinda dhidi ya majivuno pale watu wanapookoka, na dhidi ya kukata tamaa pale majibu yanapokuwa machache. Kama Paulo alivyofundisha, “Mimi nilipanda, Apolo akanywesha, bali Mungu ndiye aliyekuza” (1 Wakorintho 3:6).

Tunaamini uinjilisti si jukumu la viongozi wachache tu, bali ni wito wa kila mshirika. Kila Mkristo ni shahidi wa Kristo katika nafasi aliyo nayo, nyumbani, kazini, shuleni, na katika jamii. Ushuhuda wa kila siku, unaoambatana na tabia njema, huandaa mioyo ya watu kusikia Injili. Kanisa lina wajibu wa kuwafundisha na kuwawezesha washirika wake ili washuhudie kwa hekima, upendo, na uaminifu.

Tunaamini uinjilisti wa kweli huambatana na gharama. Kuwashuhudia watu kuhusu Kristo kunaweza kuleta kukataliwa, dhihaka, au mateso. Hata hivyo, tunakumbushwa kwamba Bwana wetu mwenyewe aliteswa, na aliwaahidi wafuasi wake kwamba watakutana na upinzani. Lakini pia aliwahakikishia uwepo wake na ushindi wa mwisho. Maandiko yanasema, “heri ninyi watakapowashutumu… kwa ajili ya jina langu” (Mathayo 5:11).

Kwa hiyo, kama kanisa, tunajitoa kwa uaminifu katika uinjilisti. Tunatangaza Kristo kwa ujasiri na upendo, tukitegemea kazi ya Roho Mtakatifu, na tukiamini kwamba Injili ina nguvu ya kubadilisha maisha. Tunaishi kama mashahidi wa nuru katika ulimwengu wa giza, tukijua kwamba kazi yetu si bure katika Bwana.

6. Utoaji wa Zaka na Sadaka kwa Uaminifu

Tunaamini utoaji ni sehemu ya ibada na uanafunzi wa Kikristo, unaotokana na neema ya Mungu na moyo wa shukrani. Utoaji hauanzi na hitaji la kanisa, bali huanza na tabia ya Mungu ambaye ni mtoaji. Mungu alitoa Mwana wake wa pekee kwa ajili ya wokovu wetu, na kwa hiyo maisha ya Mkristo huitwa kuakisi moyo huo wa kutoa. Kama Maandiko yanavyosema, “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee” (Yohana 3:16).

Tunaamini mali zote tunazomiliki zinatoka kwa Mungu, na sisi ni wasimamizi, si wamiliki wa mwisho. Hivyo, utoaji si kupoteza, bali ni kurejesha sehemu ya kile ambacho Mungu ametukabidhi. Maandiko yanatukumbusha, “Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya BWANA, Dunia na wote wakaao ndani yake.” (Zaburi 24:1). Uelewa huu hutusaidia kutoa kwa hiari na kwa uaminifu, tukijua kwamba Mungu ndiye chanzo cha mahitaji yetu yote.

Tunaamini zaka ni kanuni ya kibiblia ya uaminifu katika utoaji, iliyotolewa kama nidhamu ya kiroho ya kumheshimu Mungu kwa mali. Katika Maandiko, zaka ilieleweka kama sehemu ya kwanza ya mapato, iliyotengwa kwa ajili ya kazi ya Mungu na msaada wa huduma yake. Ingawa waamini wa Agano Jipya hawako chini ya sheria ya kulazimishwa, kanuni ya uaminifu, utaratibu, na kipaumbele katika utoaji bado inabaki kuwa ya maana. Maandiko yanasema, “Leteni zaka kamili ghalani, ili iwepo chakula nyumbani mwangu” (Malaki 3:10).

Tunaamini sadaka ni utoaji unaotolewa kwa hiari, kulingana na neema na uwezo aliopewa mtu. Sadaka huonesha moyo unaoguswa na mahitaji ya kazi ya Mungu, mahitaji ya kanisa, na mahitaji ya watu wanaoteseka. Mtume Paulo aliwahimiza waamini watoe “kila mtu kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni wala si kwa kulazimishwa” (2 Wakorintho 9:7). Hivyo, utoaji wa Kikristo hauendeshwi na hofu, bali na furaha na upendo.

Tunaamini utoaji wa kweli ni tendo la imani. Kutoa kunahitaji kumtumaini Mungu kama mpaji wa mahitaji yetu ya sasa na yajayo. Yesu mwenyewe alifundisha kwamba “kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako.” (Mathayo 6:21). Utoaji hutufundisha kuachilia tamaa ya mali, kuvunja nguvu ya fedha juu ya mioyo yetu, na kumweka Mungu mahali pa kwanza katika maisha yetu.

Tunaamini utoaji unapaswa kufanywa kwa uwazi, uaminifu, na uwajibikaji. Kanisa lina wajibu wa kusimamia rasilimali kwa hekima na uadilifu, kwa kuwa mali inayotolewa ni mali ya Bwana. Uaminifu katika matumizi ya rasilimali hujenga imani ya washirika na hulinda ushuhuda wa kanisa mbele za watu.

Kwa hiyo, kama kanisa, tunawahimiza washirika wetu kutoa kwa uaminifu katika zaka na sadaka, si kama wajibu wa kidini, bali kama mwitikio wa neema ya Mungu. Tunatoa kwa furaha, kwa shukrani, na kwa imani, tukijua kwamba Mungu “Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema.”  (2 Wakorintho 9:8).

7. Huduma na Karama za Roho Mtakatifu

Tunaamini Roho Mtakatifu huwapa waamini karama za kiroho kwa kusudi la kulijenga kanisa na kulitumikia kusudi la Mungu duniani. Karama hizi si ishara ya ukomavu binafsi wala cheo cha kiroho, bali ni zawadi za neema zinazotolewa kwa mapenzi ya Mungu kwa faida ya mwili mzima wa Kristo. Maandiko yanasema, “kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana” (1 Wakorintho 12:7). Hivyo, lengo la karama si kujitukuza, bali kujenga.

Tunaamini karama za Roho ni tofauti tofauti, lakini chanzo chake ni Roho yule yule. Kuna karama za huduma, karama za mafundisho, na karama za udhihirisho wa nguvu za Mungu, zote zikitolewa kwa kusudi moja. Maandiko yanataja karama kama hekima, maarifa, imani, uponyaji, miujiza, unabii, kupambanua roho, aina za lugha, na tafsiri za lugha (1 Wakorintho 12:8–10). Tofauti hizi zinaonesha utajiri wa neema ya Mungu ndani ya kanisa lake.

Tunaamini matumizi ya karama za Roho yanapaswa kufanyika chini ya mamlaka ya Neno la Mungu na kwa mpangilio wa kanisa. Roho Mtakatifu hapingani na Neno alilolivuvia, wala hachangii machafuko au mkanganyiko. Ndiyo maana Maandiko yanatukumbusha kwamba “Mungu si wa machafuko, bali wa amani” na kwamba mambo yote yafanyike “kwa adabu na kwa utaratibu” (1 Wakorintho 14:33, 40). Uhuru wa kiroho hauondoi hitaji la hekima na uangalizi wa kichungaji.

Tunaamini upendo ni kipimo kikuu cha matumizi sahihi ya karama zote. Bila upendo, hata karama zenye kuonekana kuwa kubwa hupoteza maana yake ya kiroho. Mtume Paulo aliweka wazi kwamba karama bila upendo ni bure, lakini upendo hujenga, huvumilia, na hutafuta mema ya wengine (1 Wakorintho 13:1–7). Hivyo, kanisa linaitwa kutanguliza tabia ya Kristo kuliko udhihirisho wowote wa karama.

Tunaamini kila mshirika ana nafasi na wajibu wa kutumika katika mwili wa Kristo. Hakuna mshirika asiye na mchango, wala hakuna karama isiyo na maana. Roho Mtakatifu humpa kila mmoja kadiri apendavyo, ili kanisa liwe mwili unaofanya kazi kikamilifu. Kama Maandiko yanavyosema, “kila kiungo, kwa kadiri kinavyopata msaada wake, huukuza mwili hata kujijenga wenyewe katika upendo” (Waefeso 4:16).

Kwa hiyo, kama kanisa, tunawahimiza washirika wetu kutambua, kukuza, na kutumia karama walizopewa na Roho Mtakatifu kwa unyenyekevu na uaminifu. Tunatoa nafasi ya huduma, tunahimiza uanafunzi, na tunasimamia matumizi ya karama kwa hekima, ili Kristo atukuzwe na kanisa lijengwe. Tunakiri kwamba kazi ya Roho Mtakatifu ni ya lazima katika maisha ya kanisa, na tunaitamani ifanyike kwa kweli, kwa mpangilio, na kwa upendo, kwa utukufu wa Mungu.

8. Kuhusu Nidhamu ya Kanisa

Tunaamini kwamba tunapaswa kufuata kwa uaminifu na kwa utaratibu hatua alizoweka Bwana Yesu katika kushughulikia makosa, kwa kuanza kumfuata ndugu aliyekosa faraghani bila kumwaibisha hadharani, tukimweleza kosa lake kwa upendo na kwa vielelezo vya Neno la Mungu, tukilenga toba na upatanisho; ikiwa hatasikia, tunapaswa kuwahusisha mashahidi wawili au watatu wenye hekima na hofu ya Mungu ili kuthibitisha jambo hilo kwa haki; na kama bado atasimama katika ukaidi, ndipo kanisa linapaswa kulishughulikia kwa uwazi na kwa heshima, si kwa jazba bali kwa roho ya haki na rehema (Mathayo 18:15-17).

Tunaamini kwamba tunapaswa kumrejesha aliyeanguka kwa roho ya upole kwa kumkaribia kama ndugu na si kama adui, tukimwombea kwa bidii, tukimfundisha kwa maandiko, tukimpa nafasi ya kusikiliza na kueleza hali yake, na tukimsaidia kuchukua hatua za toba ya kweli; katika kufanya hivyo tunapaswa kujichunguza nafsi zetu, kuepuka kiburi na roho ya kuhukumu, na kuhakikisha kuwa lengo letu si kushinda hoja bali kuokoa roho na kurudisha ushirika uliovunjika (Wagalatia 6:1).

Tunaamini kwamba tunapaswa kulinda utakatifu wa kanisa kwa kutokubali dhambi ya wazi iendelee bila kushughulikiwa, kwa kutoa maonyo ya wazi na ya haki kwa anayekosa, na pale ambapo hakuna toba, kuchukua hatua zinazofaa kama kusimamisha huduma au kumtenga kwa muda ili kanisa lisichafuliwe; tunafanya hivyo tukitambua kuwa uvumilivu kwa uovu huathiri mwili mzima, hivyo hatua hizi zinachukuliwa si kwa chuki bali kwa hofu ya Mungu na kwa kusudi la kusafisha ushirika (1 Wakorintho 5:6-7).

Tunaamini kwamba tunapaswa kupokea na kutekeleza nidhamu kama sehemu ya malezi ya kiroho, kwa kukubali maonyo ya viongozi wa kiroho, kwa kutubu pale tunapokosea, na kwa kuruhusu Neno la Mungu na uongozi wa Roho Mtakatifu kuturekebisha tabia na mwenendo wetu; tunafundishwa kwamba maumivu ya kurekebishwa si ishara ya kukataliwa bali ya upendo wa Baba anayewalea watoto wake ili washiriki utakatifu wake na kuzaa matunda ya haki katika maisha yao (Waebrania 12:6,10-11).

Tunaamini kwamba tunapaswa kuwalinda waumini dhidi ya migawanyiko kwa kumwonya kwa upendo mtu anayesababisha faraka, fitina au mafundisho ya kupotosha, tukimkemea kwa maandiko na kumwelekeza katika kweli; ikiwa ataendelea kwa ukaidi, tunapaswa kuchukua hatua ya kumtenga ili kuzuia sumu ya mgawanyiko isisambae na kuharibu umoja wa mwili wa Kristo, tukifanya yote kwa kusudi la kuokoa kanisa na kumpa nafasi ya kutafakari na kutubu (Tito 3:10-11).

MAMBO 8 KATIKA MAFUNDISHO AMBAYO HATUAMINI

Hatuamini kwamba Maandiko Matakatifu yanahitaji kuongezewa ufunuo mwingine wenye mamlaka sawa au ulio juu ya Biblia, na badala yake tunaamini Maandiko Matakatifu peke yake ni Neno la Mungu lililo kamili, la mwisho, na lenye mamlaka ya juu katika imani na maisha ya kanisa (2 Timotheo 3:16–17; Wagalatia 1:8–9; Zaburi 19:7).

Hatuamini kwamba Mungu ni nafsi moja anayejidhihirisha kwa majina tofauti kulingana na nyakati au mazingira, na badala yake tunaamini Mungu ni mmoja katika uungu wake, lakini yupo katika nafsi tatu halisi, Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu, walioungana kikamilifu katika asili na mapenzi (Mathayo 28:19; 2 Wakorintho 13:14; Yohana 1:1).

Hatuamini kwamba mwanadamu ni mwema kiasili na anahitaji tu msukumo mdogo ili kumpata Mungu, na badala yake tunaamini mwanadamu ameanguka katika dhambi, ameharibiwa kiroho, na anamhitaji Mungu amwokoe kwa neema yake (Warumi 3:10–12, 23; Mwanzo 3:1–19).

Hatuamini kwamba wokovu hupatikana kwa matendo mema, sheria, ibada, au juhudi za kidini, na badala yake tunaamini wokovu ni kwa neema ya Mungu pekee, kupitia imani katika Yesu Kristo pekee (Waefeso 2:8–9; Tito 3:5; Warumi 5:1).

Hatuamini kwamba kanisa ni taasisi ya kibinadamu inayomilikiwa au kuendeshwa kwa mamlaka ya wanadamu, na badala yake tunaamini kanisa ni mwili wa Kristo, chini ya uongozi wa Kristo mwenyewe kama kichwa chake (Wakolosai 1:18; Waefeso 1:22–23; Matendo 20:28).

Hatuamini kwamba malaika wanapaswa kuombwa, kuabudiwa, au kutafutwa kwa mawasiliano ya moja kwa moja, na badala yake tunaamini malaika ni roho/viumbe ambao ni watumishi wa Mungu walioumbwa ili kumtukuza na kutekeleza mapenzi yake chini ya mamlaka ya Kristo (Waebrania 1:14; Ufunuo 22:8–9; Wakolosai 2:18).

Hatuamini kwamba ndoa ni makubaliano ya muda kati ya watu wawili yanayofanyika kwa siri au kwa mapenzi binafsi bila msingi wa agano la Mungu (Mwanzo 2:24; Mathayo 19:6); hatuamini kwamba ndoa inaweza kujengwa nje ya mpango wa Mungu wa mwanamume na mwanamke, wala hatuamini kwamba inatosha kuthibitishwa na upande mmoja tu bila ushuhuda kamili wa kijamii, kisheria na kiroho, kwa kuwa kanuni ya uthibitisho wa mashahidi wawili au watatu ni msingi wa haki na uthabiti (Kumbukumbu la Torati 19:15); hivyo hatuamini katika ndoa isiyotambuliwa na wazazi au jamii, isiyosimama chini ya mamlaka ya serikali kama ilivyoamriwa kuhusu utii kwa mamlaka (Warumi 13:1), wala isiyobarikiwa na kanisa kama shahidi wa agano la kiroho linaloakisi uhusiano wa Kristo na Kanisa (Waefeso 5:31-32); hata hivyo, wale waliofunga ndoa kimila bila kuzingatia ushahidi huu haimaanishi kwamba wanaweza kuachana kiholela bila kufuata utaratibu wa haki na uwajibikaji, kwa kuwa agano likishawekwa lina uzito mbele za Mungu na jamii; pia hatuamini kwamba talaka ni suluhisho la kawaida la matatizo ya ndoa, kwa kuwa msimamo wa Mungu ni kuilinda ndoa na kuichukia talaka (Malaki 2:16), isipokuwa pale ambapo suluhu zote zimeshindikana kabisa na kuna tishio la maisha au madhara makubwa yasiyoweza kuzuilika, ndipo hatua za mwisho zinaweza kuchukuliwa kwa uangalifu na kwa kufuata haki.

Hatuamini katika mafundisho yanayogawanya kurudi kwa Kristo katika hatua nyingi au ufalme wa kidunia wa muda maalumu kabla ya mwisho wa historia, na badala yake tunaamini Kristo anatawala sasa, atarudi mara moja kwa utukufu, na ataleta hukumu ya mwisho pamoja na uumbaji mpya (1 Wakorintho 15:25–26; Ufunuo 1:7; Yohana 5:28–29; Ufunuo 21:1–4).

 

MAMBO 8 KATIKA MAZOEZI AMBAYO HATUAMINI

Hatuamini kwamba ibada ni burudani, onyesho, au njia ya kuamsha hisia za watu, na badala yake tunaamini ibada ni mwitikio wa heshima kwa Mungu unaojengwa juu ya Neno, maombi, na shukrani (Yohana 4:24; Wakolosai 3:16; Warumi 12:1).

Hatuamini kwamba maombi yanahitaji matumizi ya vifaa au vitu vya kidini kama maji ya upako, mafuta ya upako, chumvi ya upako, au ishara nyingine za kimwili ili yawe na nguvu, na badala yake tunaamini jina la Yesu Kristo linatosha, kwa kuwa mamlaka ya maombi iko katika Kristo mwenyewe na katika imani, si katika vitu (Yohana 14:13–14; Matendo 4:12; Wakolosai 2:9–10).

Hatuamini kwamba Mkristo anaweza kukua kiroho bila ushirika wa kanisa na waamini wengine, na badala yake tunaamini Mungu hutujenga kupitia ushirika, uwajibikaji, na maisha ya pamoja ya mwili wa Kristo (Waebrania 10:24–25; Matendo 2:42).

Hatuamini kwamba sakramenti zinafanya kazi ya kuokoa kwa zenyewe bila imani, na badala yake tunaamini sakramenti ni ishara zinazoonekana zinazothibitisha neema ya Mungu kwa wale wanaoamini Kristo (Warumi 6:3–4; 1 Wakorintho 11:26; 1 Petro 3:21).

Hatuamini kwamba uinjilisti unaweza kubadilishwa na matendo mema pekee bila tangazo la Injili, na badala yake tunaamini Injili lazima ihubiriwe kwa maneno na kuthibitishwa kwa maisha yanayoendana na kweli hiyo (Warumi 10:14–15; Mathayo 28:19–20; 1 Petro 2:12).

Hatuamini kwamba utoaji wa fedha ni njia ya kununua baraka, uponyaji, au mafanikio, na badala yake tunaamini utoaji ni ibada ya shukrani, uaminifu, na uanafunzi mbele za Mungu (2 Wakorintho 9:7; Mithali 3:9; Luka 21:1–4).

Hatuamini kwamba karama za Roho Mtakatifu zinapaswa kutumiwa kwa shinikizo au kipimo kimoja kwa waamini wote, na badala yake tunaamini Roho Mtakatifu hugawa karama, tunakiri kunena kwa lugha kama karama halali ya Roho, lakini si lazima kila muumini anene kwa lugha, kwa kuwa karama hutofautiana kwa kusudi la kulijenga kanisa (1 Wakorintho 12:7–11; 1 Wakorintho 12:29–30; 1 Wakorintho 14:26).

Hatuamini kwamba nidhamu ya kanisa ni tendo la kuwahukumu watu kwa ukali au njia ya kuwaonea waliokosea, wala si chombo cha kuwavunjia heshima au kuwaaibisha hadharani, au kuwafukuza kanisani kwa fedheha bali tunakataa mtazamo wa kuiacha dhambi iendelee bila kushughulikiwa au kuifumbia macho kwa kisingizio cha upendo usio na kweli; hatuamini katika ukimya unaolinda uovu, wala katika ukali unaokosa rehema, bali tunasimama kinyume na mwenendo wa kupuuza utaratibu wa kibiblia au kuchochea migawanyiko kwa kushindwa kuchukua hatua stahiki, kwa kuwa nidhamu ya kweli inalenga urejesho, utakatifu, na umoja wa mwili wa Kristo, si maumivu yasiyo na tumaini wala mamlaka yasiyo na upendo.

_____________________________________________________

Shekinah Presbyterian Church Tanzania

P.O.BOX 32807 Dar Es Salaam

45 Mivumoni Road, 14130 Wazo, Kinondoni, Dar Es Salaam

____________________________________________________

[1] Neno sakramenti linatokana na neno la Kilatini sacramentum lenye maana ya kiapo cha uaminifu au alama ya ahadi ambayo askari aliapa. Na baadaye katika Ukristo lililitumia kuelezea ishara zinazoonekana zilizoanzishwa na Kristo ili kuthibitisha na kueleza kwa nje neema ya ndani inayohubiriwa katika Injili.

Author
Brooklyn Simmons

Binterdum posuere lorem ipsum dolor. Adipiscing vitae proin sagittis nisl rhoncus mattis rhoncus. Lectus vestibulum mattis ullamcorper velit sed. Facilisis volutpat est velit egestas dui id ornare. Curabitur vitae nunc sed velit dignissim sodales ut eu sem. Venenatis urna cursus

Leave a Reply